Makubaliano ya Kimataifa kwa Uhamiaji ama Global Compact for Migration yaliidhinishwa wiki hiii katika kongamano la kimataifa lililofanyika mjini Marrakech, nchini Morrocco. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, makubaliano hayo ya kihistoria yanafungua njia ya kuzuia mateso na maafa kwa wahamiaji.

Jifunze zaidi kuhusu mkataba huo

Mchakato wa kuidhinisha mkataba huo ulianza miaka miwili iliyopita wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipozungumzia suala la wimbi la wahamiaji na wakimbizi, na kukubaliana kuhusu suala hilo kupitia tamko la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji lililotolewa mwezi Septemba mwaka 2016.

Mkutano wa Marrakech wa Disemba 2018 umelenga kupitisha rasmi makubaliano hayo yaliyoafikiwa na nchi wanachama 164.

Lengo la makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu uhamiaji, kulinda haki za msingi za wahamiaji na kuhakikisha wanapewa huduma za kijamii za msingi, na vilevile kulinda mipaka ya kitaifa na kuhakikisha kwamba uhamiaji unafanyika kwa njia salama na halali.

Kwa ujumla, nchi zilizotia saini Global compact for Migration zimekubaliana kuhusu malengo 23. Hapa unaweza kuyapitia kwa undani zaidi.

Kuondoa uongo na hofu kuhusu uhamiaji

Wahamiaji kwenye kambi ya wakimbizi ya Lesbos, nchini Ugiriki.

Wahamiaji kwenye kambi ya wakimbizi ya Lesbos, nchini Ugiriki.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Marrakech, Katibu Mkuu Antònio Guterres amesema kwamba kuidhinishwa kwa makubaliano hayo ni hatua ya kibinadamu, ya kibusara na yenye manufaa kwa wote, akiongeza kwamba ni aibu kujua kwamba tayari watu 60,000 wamefariki dunia tangu wakiwa katika safari ya uhamiaji.

“Mkataba huu wa uhamiaji unajikita katika masuala mawili, mosi uhamiaji siku zote umekuwa nasi, lakini ni lazima udhibitiwe na uwe salama na pili ni kwamba sera za kitaifa zinaweza kufanikiwa zaidi kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa.”[soma zaidi]

Katibu Mkuu ametaka kuondosha fikra potofu zinazoenea kuhusu Global Compact na suala la uhamiaji kwa ujumla, ya kwanza ikiwa dhana ya wengi ya kuwa makubaliano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kuamuru nchi wanachama, la si hivyo.

“Aidha, siyo kisheria. Ni mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, unaozingatia mchakato wa mazungumzo kati ya serikali kwa uaminifu”, alisisitiza Antònio Guterres, akiongeza kwamba Global Compact hautawapa wahamiaji haki za kuhamia popote wanapotaka.

Kuhakikisha haki za msingi kwa wote.

Kupitishwa kwa makubaliano hayo ambayo sasa yanajulikana kama Compact ya Marrakech yamefanyika sanjari na maadhimisho ya miaka 70 tangu kupitishwa kwa tamko la kimataifa la haki za binadamu, huku Antònio Guterres akisema “itakuwa haifai, ikiwa siku tunapoadhimisha miaka 70 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, tutaamua kwamba wahamiaji wanapaswa kutengwa kinyume na haki zinazozingatiwa kwenye tamko hili.”