Baada ya mikutano ya ngazi ya juu ya Baraza Kuu iliyofanyika mwezi Septemba, kazi za msingi zinaendelea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Kazi hizi hufanyika kupitia Kamati Kuu (Main committees) zake, ambapo maamuzi muhimu kuhusu shughuli na bajeti za shirika hili huchukuliwa. Wakati mikutano ya #UNGA hugonga vichwa vya habari kutokana na kuwepo kwa maraisi na watu maarufu katika mijadala hii, kazi za Kamati Kuu, licha ya umuhimu wake, hazijulikani sana.

Lengo la kazi za kamati kuu hizo sita ni kutafsiri dira na maazimio yanayochukuliwa katika jukwaa la Baraza Kuu kuwa hatua zinazoweza kutekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa mada zinazoangaziwa ni masuala ya ukoloni, upokonyaji silaha, ukuaji wa uchumi na usaidizi wa kibinadamu.

Kamati hizi zinafanya nini?

Kwa sababu majukumu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni mengi, kazi hizo zimegawanyika katika kamati kuu sita. Baada ya maamuzi kuchukuliwa kwa ngazi ya kamati – kupitia maafikiano (consensus) ama kura ikibidi mapendekezo yanapelekwa kwa ngazi ya Baraza Kuu kwa uamuzi wa mwisho.

Baadhi ya masuala hujadiliwa katika ngazi ya Baraza Kuu pekee, kama vile suala la Palestina.

Kuna Kamati Kuu sita za Baraza Kuu zinazoangazia mada ifuatazo:
– Kamati ya Kwanza: upokonyaji silaha na usalama wa kimataifa;
– Kamati ya Pili: masuala ya kiuchumi na kifedha
– Kamati ya Tatu: haki za kijamii, kibinadamu, haki za binadamu na masuala ya kitamaduni;
– Kamati ya Nne: hujulikana kama kamati maalum kuhusu masuala ya kisiasa na kutokomeza ukoloni;
– Kamati ya Tano: usimamizi na bajeti ya shirika;
– Kamati ya Sita: masuala ya sheria ya kimataifa.
Kila kamati inahusisha nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, na kila nchi huwa na kura moja. Kwa mujibu wa kanuni za Baraza Kuu, maamuzi ya kamati yanafanywa na wengi wa wanachama waliopo kwa kupiga kura. Wanachama wa Kamati pia wanaweza kuchukua maamuzi kwa kuafikiana.
Pamoja na Kamati Kuu sita, Baraza Kuu pia unajumuisha kamati nyingine mbalimbali, ikiwemo Kamati ya ujumla, inayosimamia shughuli za Baraza Kuu kwa ujumla.

Rais wa Baraza Kuu, Maria Fernanda Espinosa. UN Photo/Loey Felipe

Nani anafanya nini? Uongozi wa kamati

Ofisi ya kila Kamati Kuu ina Mwenyekiti mmoja, Naibu Wenyekiti watatu na Katibu mmoja – ambaye hutoa ripoti rasmi ya Kamati. Wanachaguliwa siku ya uchaguzi wa Rais wa Baraza Kuu, au wakati wa mkutano wa kwanza wa Kamati.
Kwa mujibu wa kanuni za Baraza Kuu, mwenyekiti wa Kamati Kuu hawezi kupiga kura, ila mjumbe mwingine wa nchi yake anaweza kupiga kura kwa niaba yake.
Wenyekiti wa kamati kuu pia ni wajumbe wa Kamati ya Jumla, inayoongozwa na Rais wa Baraza Kuu.

 

Wawakilishi wa Ufalme wa Eswatini. Kila nchi mwanachama huwa na kura moja kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. UN Photo/Cia Pak