Viongozi wa Palestina, Israel na Comoro waongea kwenye siku hii ndefu ndani ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ukatili wa kijinsia ni baadhi ya mada zilizozungumzwa pia.

  • Magonjwa yasiyo yakuambukizwa husababisha asilimia 70 ya vifo duniani

Takwimu hiyo ya kushtua imekuwa mada ya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu NCDs, yaani magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Lengo lilikuwa ni kujadiliana kuhusu namna ya kutokomeza magonjwa hayo yakiwemo maradhi ya moyo, kiarusi, saratani ya matiti au kisukari.  Miongoni mwa maamuzi yaliyochukuliwa ni kuongeza kodi juu ya sigara, pombe na vyakula venye sukari, kudhibiti uvutaji sigara hadharani na kukataza matangazo ya vileo.

Katika ujumbe wake Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed amesema utandawazi, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi ya watu wanaoishi mijini ni aina mbalimbali za mabadiliko yanayosababisha magonjwa hayo kuzidi kuenea na kuwa mzigo kwa jamii. Soma zaidi.

  • Habari njema za haki za binadamu

Katika maadhimisho ya miaka 70 ya haki za binadamu, mradi mpya umezinduliwa kwa ajili ya kusambaza “habari njema za haki za binadamu”, Katibu mkuu akisisitiza kwamba hakuna usalama endelevu bila kuheshimu haki za binadamu kwa wote.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi Michelle Bachelet ametoa mfano wa habari njema kuhusu haki za binadamu, moja ikiwa ni maridhiano kati ya nchi za Eritrea na Ethiopia akisema:

Baada ya miaka 20 ya  uhasama nimefurahia jinsi watu wa mataifa hayo walivyopokea kwa furaha makubaliano hayo na ni kwa sababu nzuri.Matokeo ya haraka ni kurejelea mawasiliano ya simu , safari za ndege , na viongozi wa mataifa hayo mawili kuahidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisasia wa nchi hizo na kuona kama maendeleo ya amani na ushirikiano zaidi vinatanda katika eneo zima la pembe ya Afrika.”

Soma zaidi.

  • Spotlight yalenga kukomesha mauaji ya wanawake

Mkakati mpya wa kusitisha mauaji ya wanawake na wasichana katika nchi zilizo Amerika ya Kusini umezinduliwa pia leo. Mkakati huo uitwao Spotlight umefadhiliwa kwa kiasi cha euro milioni 50 kwa ajili ya kuchagiza mtazamo mpya kuhusu usawa wa kijinsia, kusaidia manusura na kuimarisha taasisi na sheria.

Soma zaidi.

  • Viongozi 39 wahutubia baraza kuu

Katika siku hiyo ya tatu ya mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, marais na mawaziri 39 walikuwa wameratibiwa katika orodha ya hotuba. Miongoni mwao walikuwa ni Waziri Mkuu wa Uganda Ruhakana Rugunda, na Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Augustine Mahiga.

Rais wa Comoro Azali Assoumani yeye amezingatia umuhimu wa kuleta mabadiliko ndani ya Umoja wa Mataifa, akisisitiza pendekezo la kuteua nchi mbili za Afrika kupata viti vya kudumu kwenye Baraza la Usalama.

Walioongea pia ni Waziri Mkuu wa Israel, ambaye ameonyesha picha ya kile anachodai ni pahali ambapo pamefichwa vifaa vya nyuklia huko Tehran, mji mkuu wa Iran. Kwa upande wake rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesema kuwa hawatakubali usuluhishi wa Marekani pekee katika mchakato wa kuleta amani akisema ni kwa sababu utawala wa Marekani umepoteza uhalali katika mgogoro huo wa mashariki ya kati kutokana na matukio ya hivi karibuni.

Maelezo mengine hapa