Kutoka silaha za nyuklia hadi ugonjwa wa TB, vikaragosi na waigizaji filamu…  Makao makuu ya Umoja wa Mataifa yalipamba moto.

  • Marais wameendelea kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Jumatano tarehe 26 ilikuwa ni siku ya pili ya mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Baada ya marais 35 kuongea jumanne, leo 39 wamefuatana siku nzima, wakiwemo Uhuru Kenyatta wa Kenya na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Ikiwa ni bara ambalo lina idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, Afrika ina uwezo wa kukua na kuibuka lango lijalo la ukuaji wa uchumi duniani,” amesema Rais Ramaphosa.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema wananchi wanazidi kupoteza imani kwa serikali zao, kutokana na kuenea kwa vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma.

  • Donald Trump aongoza mkutano kuhusu majaribio ya silaha za nyuklia.

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa dhidi ya majaribio ya silaha za nyuklia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba zaidi ya majaribio 2,000 ya nyuklia yameshafanyika na kuathiri watu wengi, hasa wanoishi kwenye mazingira magumu. Akifungua mjadala wa ngazi ya juu uliofanyika kwa ajili ya siku hiyo, rais Donald Trump wa Marekani ametoa wito kuhusu Iran:

“Nawaomba wajumbe wote wa baraza la Usalama kushirikiana na Marekani kuhakikisha utawala wa Iran unabadili mwelekeo wake , na kuhakikisha asilani haitomiliki bomu la nyuklia.”

Wajumbe wote wameafikiana kuwa kupinga kuenea kwa silaha za maangamizi sio chaguo ni lazima. Soma Zaidi.

  • Azimio lapitishwa kuhusu kutokomeza kifuaa kikuu – TB

Leo pia mkutano wa ngazi ya juu umefanyika na kuongozwa na mkuu wa Shirika la afya duniani WHO na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed.

Bi Mohammed amesema usugu wa dawa za TB unakadiriwa kusababisha theluthi moja ya vifo vitokanavyo na usugu wa dawa duniani. Ameongeza kwamba jukumu la Umoja wa Mataifa katika kutokomeza TB ni la dharura na kwamba ugonjwa huu mbaya unagusa kila bara na kila nchi. Tayari takribani watu milioni 10.4 wameambukizwa. Soma zaidi.

  • Kutoka studio ya mitandao ya kijamii

Watu mashuhuri walitembelea studio wetu, wakiwemo mwigizaji filamu Winston Duke wa filamu ya Black Panther. Alitoa ujumbe wake: “Mapambano ya usawa wa kijinsia ni mapambano yetu sote”.

 

Tumefurahia kumhoji waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Bi. Monica Juma, ambaye amesisitizia umuhimu wa kushirikisha vijana katika ngazi zote za uongozi.

Pia kiragosi Raya wa Sesame Street akileta ujumbe muhimu kuhusu upatikanaji maji safi na sabuni ili kuzuia magonjwa.

  • Yatakayojiri alhamis kwenye Umoja wa Mataifa

Mjadala wa wazi wa kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utaendelea na hotuba za marais na mawaziri wakiwemo wa Uganda na Tanzania. Usikose kuzifuatilia mbashara hapa.

Siku ya utalii duniani itaadhimishwa pia siku ya alhamis kwa kumulika umuhimu wa kuchchea utalii endelevu kwa ajili ya kunufaisha jamii na kutunza mazingira.

 

Maelezo mengine hapa