1. Hotuba ndefu zaidi iliyotolewa kwenye Umoja Wa Mataifa?

Kwa mujibu wa Kitabu cha Guinness World Records, hotuba kubwa zaidi iliyowahi kutolewa kwenye mikutano ya Umoja wa Mataifa ni ya V.K. Khrishna Menon kutoka India, mwaka 1957. Yaripotiwa kuwa alilazwa hospitalini baada ya kuhutubia kwa muda wa masaa matano, na kuendelea na hotuba kesho yake kwa muda wa masaa mengine matatu.

Hotuba ndefu zaidi pia zilizoorodheshwa na ripoti za Umoja wa Mataifa ni:

  • Fidel Castro wa Cuba aliongea kwa dakika 269 yaani karibu masaa nne na nusu mwaka 1960;
  • Sékou Touré wa Guinea aliongea kwa dakika 144 (masaa mawili na dakika 24) mwaka 1960;
  • Nikita Krushchev wa Urusi, dakika 140 mwaka 1960;
  • Soekarno wa Indonesia, dakika 121 mwaka 1960;
  • Muammar Al-Qadhafi wa Libya kwa dakika 96 mwaka 2009.

Siku hizi ni maadili kwa viongozi wanaohutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutozidi dakika 15.

2. Ni lini Bw. Khrushchev alipiga meza na kiatu chake?

Tukio hilo lilitokea tarehe 12, Oktoba, mwaka 1960. Aliyekuwa kiongozi wa Umoja wa Kisovyeti (USSR, sasa Urusi) alikuwa akibishana na rais wa Ufilipino kuhusu umuhimu wa kuwapatia uhuru nchi zilizotawaliwa na wakoloni. Tukio hilo halikurekodiwa kwenye muhtasari rasmi wa mkutano ila kwenye ripoti ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na gazeti mbalimbali. (A/PV.902).

3. Je Baraza Kuu limewahi kujadili kuhusu vitu vya angani visivyotambuliwa?

Mwaka 1977 na 1978, ombi hilo lilitolewa na nchi ya Grenada. Lengo lilikuwa ni kuunda shirika au idara maalum kwa ajili ya kuratibu na kusambaza utafiti kuhusu  vitu vya angani visivyotambuliwa yaani UFOs.

Lakini maazimio hayo hayakupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. (p. 237 – A/33/45).

4. Je kuna jeshi la Umoja wa Mataifa?

 

Hapana, Umoja wa Mataifa hauna jeshi lake lenyewe. Ila kuna jeshi na polisi 110,000 wanaolinda amani kote duniani katika operesheni 14 za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.

Walinda amani hawa ni jeshi na polisi wa nchi zao binafsi. Nchi hizi huchangia katika operesheni za ulinzi wa amani. Walinda amani wanavaa sare za nchi yao, isipokuwa kofia ya blu ya Umoja wa Mataifa.

Soma zaidi hapa: https://peacekeeping.un.org/en

5. Je kuna wimbo wa Umoja wa Mataifa?

Hapana, hakuna wimbo rasmi wa Umoja wa Mataifa. Ila mwaka 1971, tarehe 24, Oktoba, 1971, wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya Umoja wa Mataifa, Pablo Caslas wa Hispania alitunga wimbo ulioitwa “A hymn to the UN”, mistari ikiwa ni ya mshairi W.H. Austen kutoka Uingereza.

Isome hapa:

https://ask.un.org/loader.php?fid=8268&type=1&key=ab03bbab47193e04dc3c58218191ff5a

6. Asili ya kofia za blu za walinda amani wa Umoja wa Mataifa?

Umoja wa Mataifa ulipoundwa, kanuni zilikuwa zikiamuliwa kadri zikihitajika. Mwaka 1947, azimio 167 liliamulia kutumia rangi ya blu kwa bendera ya Umoja wa Mataifa. Mwaka 1948, vikosi vya kwanza vya ulinzi wa amani vilipopelekwa nchini Misri, ikabidi kutafuta kofia za kipekee zinazoweza kubainisha walinda amani kutoka kwa jeshi wengine. Hakukuwa na muda wa kutengeneza kofia maallum kwa hiyo walitumia kofia nyeupe za jeshi la Marekani na kuzipaka rangi ya blu ya Umoja wa Mataifa.

7. Jiwe la msingi la jengo la Umoja wa Mataifa mjini New York liko wapi?

Jiwe la msingi limewekwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, chini ya jengo la mkataba. Neno “Umoja Wa Mataifa” limechongwa kwenye jiwe lile katika lugha tano rasmi za wakati ule (kiingereza, kifaransa, kirusi, kichina na kihispania), pamoja na MCMXLIX, ikimaanisha mwaka 1949 kwa mfumo wa kirumi. Pia ndani ya jiwe lile kuna sanduku lenye tamko la kimataifa la haki za binadamu na mkataba wa Umoja wa Mataifa. Jiwe la msingi liliwekwa wakati wa hafla maalum iliyofanyika tarehe 24, Oktoba, 1949, miaka minne baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa.

8. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limewahi kukutana nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa?

Kabla ujenzi wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa haujakamilika, mikutano ya Baraza Kuu ilikuwa ikifanyika London, Paris na kwenye eneo la Flushing Meadows mjini New York. Kikao cha kwanza cha Umoja wa Mataifa, mwaka 1946, kilifanyika mjini London, Uingereza.

9. Historia ya bendera la Umoja wa Mataifa?

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 167 kuhusu bendera yake tarehe 20, Oktoba, mwaka 1947. Nembo la Umoja wa Mataifa ni ya rangi nyeupe juu ya rangi ya blu. Azimio hilo hilo pia likaamulia kuwa kila tarehe 24, Oktoba itakuwa ni siku ya Umoja wa Mataifa.

http://www.un.org/ga/search/view_doc.asp?symbol=A/RES/167(II)

10. Je Umoja wa Mataifa uliwahi kupewa tuzo la amani la Nobel?

Mwaka 2001, Umoja wa Mataifa ulipewa tuzo ya amani ya Nobel pamoja na Kofi Annan aliyekuwa Katibu Mkuu wakati ule.

Lakini baadhi ya viongozi wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake waliwaji kupewa tuzo hiyo, wakiwemo Dag Hammarskjöld, baada ya kifo chake mwaka 1961, Ralph Bunche, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Palestina mwaka 1950, Mohamed ElBaradei, Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la atomiki, IAEA mwaka 2005, Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR mwaka 1954 na 1981, na mengine mengi.

Taarifa hizo hupatikana kwenye tovuti ya http://ask.un.org/