Kama uliwahi kufuatilia mijadala ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, utakuwa umeshaona kwamba baada ya uamuzi wowote, Rais wa Baraza Kuu anapiga rungu. Rungu hilo lenye umbo lisilo la kawaida ni zawadi kutoka kwa Iceland, na historia yake ni ya ajabu…

Iceland inajulikana kama demokrasia kongwe zaidi duniani. Ncini humo, mkutano wa kwanza wa aina ya kisasa ya bunge ulifanyika mwaka 930. Ndio maana Iceland ikapendekeza rais wa “bunge la kimataifa” atumie  rungu kutoka kwao.

Kwenye mikutano ya Umoja wa Mataifa, rungu hutumiwa kufungua na kufunga mikutano, kuchagua viongozi, kupitisha maazimio ama kuleta utulivu.

UN Photo/Mark Garten.
Pichani ni Joseph Deiss, Rais wa Baraza Kuu, mwaka 2012, akipiga rungu baada ya Baraza Kuu kumteua Ban Ki Moon kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa awamu ya pili.

Rungu lapewa jina la rungu la Thor

Mwaka 1952, jengo mpya la makao makuu ya Umoja wa Mataifa lilipozinduliwa, aliyekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa kwanza wa Iceland, Bw. Thor Thors, akampatia
rais wa Baraza Kuu rungu kubwa. Rungu lile lenye umbo la silaha za zamani za maharamia wa Skandinavia (Vikings) likapewa jina la utani la Rungu la Thor.

Rungu la vunjika…

Oktoba mwaka 1960, vurugu zikajaa kwenye kikao cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Aliyekuwa Rais ya USSR (Urusi sasa), Nikita Kruschchev, akapiga kiatu chake juu ya
meza. Kutuliza makelele yaliyofuata tukio hilo, Rais wa Baraza Kuu, Frederick Boland, akapiga rungu mara kadhaa hadi likavunjika! Umoja wa Mataifa ukaiomba Iceland ichonge rungu lingine lenye kufanana kabisa lile
lililovunjika.

.. na kupotea

Bado isitoshe! Rungu likadumu bila kuvunjika tena, lakini mwaka 2005, likapotea! Ombi lingine likatolewa kwa Iceland ichonge rungu lingine. Mara hii, msaani maarufu Sigridur Kristjandottir akapewa jukumu hilo kwa kuzingatia uimara wa nyenzo.

UN Photo/Manuel Elias. Rais wa kikao cha 72 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Miroslav Lajčák, amkabidhi “Rungu la Thor” Bi. Maria Fernanda Espinosa Garcés, anayeongoza kikao cha 73 cha Baraza Kuu.

Utawala wa sheria

Pamoja na umbo lake imara na la kipekee, rungu la Baraza Kuu linabeba ujumbe maalum. “Jamii inapaswa kujengwa kwenye msingi wa sheria” ni maneno yaliyochongwa juu yake kwa Kilatini na Kiaislandi. Licha ya kufanana na silaha ya maharamia wa Skandinavia waliokuwa wakitumia jehuri kuzishinda nchi zingine, ndani ya Baraza Kuu, rungu hilo la Thor hutumiwa kuleta amani na mshikamano baina ya mataifa ya dunia!